Imeandikwa na David Simons, Pennsylvania State University; Ayşegül Bakır, Hacettepe University, Türkiye; Johanna Nurmi, University of Helsinki, Finland
Kwa kawaida, COVID-19 huandikwa kana kwamba ni jambo la zamani na hutajwa tu kama maambukizi ya mfumo wa upumuaji. Hata hivyo, COVID-19 bado ni kichocheo kikali cha mfadhaiko wa mwili mzima, hasa kwa wagonjwa walio katika hatari kubwa wenye magonjwa sugu ya moyo, kimetaboliki, kinga au mfumo wa upumuaji. Hatari haitokani tu na virusi vyenyewe; bali pia na mfululizo wa mabadiliko ya mwili yanayoweza kusababisha kushindwa kwa viungo.
Kama wataalamu wa afya, tunaifahamu vizuri safari ya kitabibu ya ugonjwa huu. Mgonjwa mwenye chronic obstructive pulmonary disease (COPD) au ugonjwa sugu wa tishu za mapafu huwa katika hatari kubwa sana ya kupata Acute Respiratory Distress Syndrome (ARDS). Hatari hii huongezeka zaidi kwa wagonjwa wenye matatizo ya kimetaboliki; kwa mfano, wagonjwa wenye kisukari kisichodhibitiwa au unene uliokithiri huwa tayari wana uvimbe wa muda mrefu na matatizo ya mishipa midogo, hali inayouandaa mwili kwa mwitikio mkali wa uchochezi. Kwa hivyo, uvimbe wa mwili mzima unaosababishwa na COVID-19 unaweza kuchochea kwa urahisi kushindwa kwa moyo, vifungo vidogo vya damu mwilini, au kuharibika ghafla kwa figo.
Kwa watu wenye kinga dhaifu, mwitikio usiodhibitika wa kinga na muda mrefu wa kutoa virusi mwilini huongeza hatari ya kupata maambukizi ya ziada ya bakteria, na hivyo kuzidisha ukali wa hali yao. Pia tunaona ongezeko la matatizo ya neva kama vile acute encephalopathy na kuchanganyikiwa (delirium). Haya ni hatari zaidi kwa wazee, kwani mara nyingi husababisha kushuka kwa uwezo wa kufanya shughuli za kila siku (ADLs), kupoteza uhuru, na kuhitaji kulazwa hospitalini kwa dharura pamoja na uangalizi wa muda mrefu.
Mzigo wa matatizo haya hauishii kwa mgonjwa mmoja tu. Mzee anayepoteza uwezo wake wa kawaida kutokana na delirium, au mgonjwa mwenye kinga dhaifu anayepata nimonia ya bakteria, hahitaji tu kulazwa kwa muda mfupi. Wanahitaji huduma za dharura za kiwango cha juu, usimamizi wa kitaalamu kutoka fani mbalimbali, na mara nyingi ukarabati wa muda mrefu. Hii huathiri mfumo mzima wa afya: vitengo vya wagonjwa mahututi na wodi za wazee hujaa, upasuaji wa hiari huahirishwa, na huduma kwa wagonjwa wengine wenye magonjwa sugu hukatika.
Zaidi ya hayo, shinikizo la kudumu la kushughulikia madhara haya yanayoweza kuzuilika, pamoja na changamoto za kuwaandaa wagonjwa waliopoteza uwezo wao wa kujitegemea kurudi nyumbani, linaweza kuchangia uchovu wa kazi na majeraha ya kimaadili (moral injury) kwa wahudumu wa afya. Majeraha ya kimaadili hutokea pale mtu anapolazimika kufanya mambo yanayopingana na maadili au misingi yake ya kitaaluma. Uchovu wa kazi (burnout) hutokana na mkusanyiko wa msongo wa kazi, kuchoka kiakili, kupoteza imani katika uwezo binafsi, na kujitenga kijamii. Hali hizi mbili huongeza wasiwasi, huzuni, dalili za mwili, na huathiri moja kwa moja usalama wa mgonjwa, nia ya kuendelea na taaluma, na ubora wa huduma.
Daraja la kitabia
Mara nyingi, pengo kati ya maambukizi mepesi ya awali na kulazwa hospitalini hutokana na tabia. Kwa nini wagonjwa walio katika hatari kubwa wanachelewa kutafuta huduma au kukataa dawa za mapema za kupunguza makali ya virusi na kurekebisha kinga wakati ndizo zina ufanisi zaidi?
Utafiti wa kisaikolojia unaonyesha kuwa wagonjwa mara nyingi hukadiria vibaya hatari zao katika hatua za mwanzo za ugonjwa. Mgonjwa mwenye kinga dhaifu anaweza kupata kikohozi chepesi na kudhani ni mafua ya kawaida, bila kutambua dirisha dogo la muda lililopo la kuzuia matatizo makubwa. Vivyo hivyo, mzee anayeanza kuonyesha dalili za delirium hawezi kutathmini kwa usahihi hali yake wala kutafuta msaada.
Aidha, upendeleo wa kiakili na kihisia katika kutathmini hatari unaweza kuchelewesha hatua. Kwa mfano, mgonjwa mwenye kushindwa kwa moyo anaweza kuzoea maumivu ya kifua ya muda mrefu na hivyo kupuuza maumivu mapya yanayosababishwa na COVID-19. Wengine hukataa ukweli kwa sababu ya woga wa kukabiliana na tishio jipya, au huonyesha matumaini yasiyo ya kweli wanapokuwa na dalili nyepesi, bila kutambua kuwa wako katika kundi la hatari.
Kuchelewa kukubali matibabu bado ni jambo la kawaida. Wagonjwa wanaweza kukosa kuamini dawa mpya, kupunguza uzito wa dalili zao ili kuepuka kuwa “mzigo,” au kuhisi kuzidiwa na ugumu wa kufuata hatua za kupata huduma.
Maarifa ya kitabibu pekee hayawezi kuziba pengo hili. Ili kupunguza kulazwa hospitalini kunakoweza kuzuilika na kulinda uwezo wa mfumo wa afya, tunahitaji kuunganisha sayansi ya tabia katika mashauriano yetu ya kila siku. Tunahitaji kubadili mtazamo kutoka kutoa taarifa tu za kitabibu hadi kuwezesha mabadiliko ya tabia kwa mgonjwa na mlezi.
Kwa kutumia Mbinu Maalum za Kubadili Tabia (Behaviour Change Techniques – BCTs), wagonjwa walio katika hatari kubwa na mitandao yao ya msaada wanaweza kuhamasishwa kuchukua hatua mapema kabla hali haijawa mbaya. Mtazamo huu wa mapema huwafanya wagonjwa na walezi kuwa washiriki hai katika ufuatiliaji wa afya yao, na hivyo kulinda uwezo wa mfumo wa afya.
Mapendekezo ya vitendo
- Mpango wa “Siku za Ugonjwa” Epuka ushauri wa jumla kama “Piga simu ukizidiwa.” Wagonjwa walio katika hatari kubwa, hasa wazee wanaoweza kupata delirium, wanahitaji viashiria vya wazi na vinavyopimika. Andika mpango mahsusi wenye viashiria vya kupumua, utambuzi na usimamizi wa kisukari, na hakikisha mgonjwa na mlezi wanaweza kutumia vifaa vya ufuatiliaji nyumbani.
- Kubinafsisha hatari ili kupunguza kusitasita Badala ya ujumbe wa jumla kama “COVID-19 ni hatari,” elekeza hatari moja kwa moja kwenye ugonjwa sugu wa mgonjwa ili kuongeza uelewa na umuhimu wa kuchukua hatua mapema.
- Kuwasha mfumo wa msaada wa kijamii Tambua mtu wa msaada ambaye atamsaidia mgonjwa akipata matokeo chanya ya COVID-19. Hii ni muhimu sana kwa wazee na wagonjwa wenye kupungua kwa uwezo wa utambuzi.
Imetafsiriwa na Mercy Mukoya