Practical Health Psychology

Translating research to practice, one blog post at a time

Practical Health Psychology
Kuishi Baada ya COVID-19: Kusimamia Athari za Kiafya za Muda Mrefu

Kuishi Baada ya COVID-19: Kusimamia Athari za Kiafya za Muda Mrefu

Imeandikwa na Dominika Kwasnicka, University of Melbourne, Australia and Rizmina Rilwan, Independent Researcher from Sri Lanka

COVID-19 baada ya awamu ya papo hapo: kile bado tunajifunza

Ingawa awamu ya papo hapo ya COVID-19 imekuwa lengo la tahadhari ya kimataifa, matokeo yake ya muda mrefu yanazidi kutambuliwa katika huduma za afya. WHO inabainisha baadhi ya watu kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kupata athari za muda mrefu za COVID-19 baada ya kuambukizwa virusi vya SARS-CoV-2. Hii inajumuisha wanawake, watu wazima wenye umri mkubwa, wavutaji sigara, watu wenye uzito kupita kiasi au unene uliopitiliza, wale walio na magonjwa sugu yaliyokuwepo kabla ya kuambukizwa, pamoja na watu wenye ulemavu. 

Watu wengi huendelea kuwa na dalili wiki au miezi baada ya kuambukizwa, huku wengine wakipata magonjwa mapya au kuzorota kwa hali zao sugu. Kuelewa athari hizi za muda mrefu ni muhimu ili kutoa huduma inayomlenga mgonjwa, hasa kwa wazee na wale walio tayari katika hatari ya magonjwa sugu. Kwa watoa huduma za afya, hili linahitaji mabadiliko kutoka usimamizi wa papo hapo hadi ufuatiliaji wa muda mrefu, kuzuia madhara, na upangaji wa huduma unaoratibiwa. 

Long COVID ni nini? Kuelewa hali changamano inayobadilika 

Long COVID, inayojulikana pia kama hali ya baada ya COVID-19, hufafanuliwa kama kuendelea kwa dalili au kuibuka kwa dalili mpya miezi 3 baada ya maambukizi ya awali ya SARS-CoV-2, na dalili hizi kudumu kwa angalau miezi 2 bila sababu nyingine inayoeleweka (hii ni fasili ya WHO; mashirika mengine yana tofauti ndogo). Dalili za kawaida ni uchovu, upungufu wa pumzi, changamoto za utambuzi (“brain fog”), maumivu ya kifua, na matatizo ya usingizi. Dalili zinaweza kubadilika-badilika na mara nyingi huathiri viungo mbalimbali. Wahudumu wa afya wanapaswa kutambua kuwa dalili mara nyingi si maalum na zinaweza kuhitaji uchunguzi mpana unaozingatia mifumo ya mwili. 

Makadirio ya maambukizi hutofautiana, lakini Long COVID inaonekana kuwa ya kawaida zaidi kwa wazee, watu wenye magonjwa sugu, na wale waliopata ugonjwa mkali hapo mbeleni. Hata hivyo, inaweza pia kuwapata watu waliokuwa na maambukizi mepesi au bila dalili, jambo linaloifanya kuwa hali pana na isiyotabirika. 

Jinsi COVID-19 inavyobadilisha hatari ya magonjwa sugu

Ushahidi unaojitokeza unaonyesha kuwa COVID-19 imehusishwa na kuibuka au kuzorota kwa magonjwa sugu. Kwa mfano, baadhi ya wagonjwa hupata kisukari kipya baada ya maambukizi, huenda kutokana na athari za virusi kwenye kongosho au mabadiliko ya kimetaboliki yanayohusiana na uvimbe. Vivyo hivyo, matatizo ya moyo kama kuumia kwa misuli ya moyo, mapigo yasiyo ya kawaida, na hatari kubwa ya kushindwa kwa moyo yameripotiwa hata baada ya kupona awamu ya papo hapo. Ufuatiliaji wa mara kwa mara wa viashiria vya hatari ya magonjwa ya moyo na metaboli ni sehemu muhimu ya huduma baada ya COVID. 

Mambo haya yanaonyesha umuhimu wa kuiona COVID-19 si tu kama maambukizi ya kupumua ya papo hapo, bali kama hali yenye athari za kimfumo na za muda mrefu. Kwa wagonjwa wenye magonjwa sugu, COVID-19 inaweza kuharakisha maendeleo ya ugonjwa au kufanya usimamizi wake kuwa mgumu zaidi. 

Wazee baada ya COVID-19: Kusimamia nafuu, kudorora, na uimara 

Wazee wameathirika zaidi na athari za papo hapo na za muda mrefu za COVID-19. Watu wenye umri wa miaka 65 na zaidi wana uwezekano mkubwa wa kupata dalili na matatizo ya Long COVID kuliko watu wazima vijana. Zaidi ya hayo, COVID-19 inaweza kuchochea au kuzidisha magonjwa sugu kama ya moyo, mapafu, na matatizo ya mfumo wa neva. 

Zaidi ya matatizo ya kiafya, wengi hupata kupungua kwa uwezo wa kufanya shughuli, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa uwezo wa kutembea, udhaifu wa misuli, na kupoteza uhuru wa kujihudumia. Kutengwa kijamii wakati na baada ya ugonjwa kunaweza kuongeza hatari ya kupungua kwa uwezo wa kiakili na changamoto za afya ya akili kama msongo wa mawazo na wasiwasi. Ubora wa maisha mara nyingi hupungua kwa kiasi kikubwa. Hata baada ya kuonekana kupona, wagonjwa wazee wanaweza kushindwa kurudi katika kiwango chao cha awali cha utendaji, na hivyo kuhitaji msaada zaidi kutoka kwa wahudumu wa afya, walezi, na huduma za jamii. Tathmini ya mara kwa mara ya uwezo wa kufanya shughuli, afya ya akili, na usaidizi wa kijamii ni muhimu sana kwa kundi hili.

Kwa nini Long COVID inahitaji huduma ya pamoja na ya muda mrefu 

Kutokana na wigo mpana wa matatizo ya baada ya COVID, mbinu ya huduma inayojumuisha wataalamu mbalimbali ni muhimu. Hii inaweza kujumuisha madaktari wa huduma ya msingi, wataalamu (kama madaktari wa moyo au wa homoni), wataalamu wa mazoezi ya viungo, wanasaikolojia, na wataalamu wa ustawi wa kijamii. Ufuatiliaji wa mara kwa mara huruhusu utambuzi wa mapema wa hali mpya au zinazozorota na kuwezesha hatua za haraka. Kuanzisha njia wazi za rufaa na mawasiliano kati ya huduma mbalimbali kunaweza kuboresha mwendelezo wa huduma. 

Huduma inapaswa pia kuzingatia mahitaji ya mtu mmoja mmoja. Wagonjwa wenye Long COVID mara nyingi huwasilisha dalili nyingi zinazofuatana, na safari yao ya kupona hutofautiana sana. Kujumuisha masuala ya Long COVID katika mipango ya usimamizi wa magonjwa sugu kunaweza kuboresha matokeo na kupunguza hatari ya matatizo zaidi. Kushirikiana katika kufanya maamuzi na kuweka malengo husaidia kuhakikisha huduma inalingana na vipaumbele na uwezo wa mgonjwa. 

Kuangalia mbele: Kujenga uelewa, kujiamini, na mwendelezo wa huduma Wahudumu wa afya wana jukumu muhimu katika kutambua na kushughulikia athari za muda mrefu za COVID-19. Kuongeza uelewa kwa wagonjwa, kuthibitisha dalili zao, na kutoa mwongozo wazi kunaweza kupunguza wasiwasi na kuongeza ushiriki wao katika huduma. Kujiamini katika kujadili Long COVID na wagonjwa ni sehemu muhimu ya mazoezi ya kitabibu. Kadiri utafiti unavyoendelea kubadilika, ni muhimu kubaki na taarifa mpya na kuwa tayari kurekebisha mbinu. Mzigo wa muda mrefu wa COVID-19 huenda ukaendelea kwa miaka, na hivyo kuwa sehemu muhimu ya usimamizi wa magonjwa sugu kwa muda mrefu. Elimu endelevu ya kitaaluma (ikiwemo mafunzo haya) na kujumuisha ushahidi mpya katika mazoezi kutakuwa muhimu ili kuboresha matokeo ya wagonjwa. 

Mapendekezo ya kiutendaji

  1. Uliza kwa makusudi kuhusu dalili zinazoendelea 

Wakati wa mashauriano ya kawaida, waulize wagonjwa kuhusu dalili zinazoendelea baada ya COVID-19, hata kama maambukizi ya awali yalikuwa mepesi. Uchovu, upungufu wa pumzi, na mabadiliko ya utambuzi mara nyingi hayatajwi. Maswali mahususi huruhusu utambuzi wa mapema, tathmini kwa wakati, na rufaa inapohitajika.

  • Chunguza uwepo wa magonjwa mapya au kuzorota kwa yale ya awali 

Fuatilia dalili za kisukari kipya, matatizo ya moyo, au kuzorota kwa hali zilizokuwepo. Hii inaweza kujumuisha kupima sukari ya damu, shinikizo la damu, na dalili za moyo. Kujumuisha uchunguzi huu katika ufuatiliaji wa baada ya COVID kunaweza kusaidia kugundua matatizo mapema.

  • Saidia urejeshaji wa uwezo wa kufanya shughuli kwa wazee

Hamasisha kurejea taratibu katika shughuli za mwili kulingana na uwezo wa mgonjwa. Mpango wa ukarabati na shughuli unapaswa kuzingatia mtu mmoja mmoja, kwani baadhi ya wagonjwa hupata kuongezeka kwa dalili baada ya kufanya shughuli kupita kiasi. Kuwapeleka kwa wataalamu wa mazoezi ya viungo au huduma za ukarabati kunaweza kusaidia kuboresha uwezo wa kutembea, nguvu, na uhuru. Pia zingatia uchunguzi wa uwezo wa kiakili na afya ya akili, hasa kwa wale waliotengwa kwa muda mrefu.

  • Tumia mbinu ya huduma ya pamoja

Ratibu huduma kati ya taaluma mbalimbali inapowezekana. Wagonjwa wenye dalili changamano au zinazoendelea wanaweza kufaidika na mchango wa pamoja kutoka huduma za kitabibu, afya saidizi, na ustawi wa kijamii. Mawasiliano wazi kati ya watoa huduma ni muhimu ili kuepuka huduma iliyogawanyika.

  • Toa faraja na uweke matarajio halisi 

Kupona kutokana na Long COVID kunaweza kuwa kwa polepole na kwa viwango tofauti. Tambua wasiwasi wa mgonjwa, thibitisha uzoefu wao, na toa taarifa wazi kuhusu wanachoweza kutarajia. Kusaidia mikakati ya kujisimamia na ufuatiliaji wa mara kwa mara kunaweza kuwasaidia wagonjwa kuhisi wana udhibiti zaidi wa safari yao ya kupona.

Imetafsiriwa na Mercy Mukoya

Practical Health Psychology

Translating research to practice, one blog post at a time

Subscribe

Sign up today to get notified whenever a new blog post is published!

And don’t worry, we hate spam too! You can unsubscribe at anytime.